Mtoto mwenye umri wa siku nane, ameibwa baada ya mama yake kunyweshwa juisi inayosadikiwa kuwa na dawa za kulevya.
Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Dk. Nassoro Mzee,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mwanamke huyo, Teddy
Bishaliza (19), alilazwa katika Wodi 17 kufuatia afya yake kuathiriwa
na dawa hizo, huku mtoto wake wa kike ikidaiwa kuwa aliibwa katika tukio
lililotokea juzi mtaa wa Chidachi, Manispaa ya Dodoma.
Akizungumza
kwa tabu wodini hapo, Bishaliza alisema alijifungua mtoto huyo Jumatano
ya wiki iliyopita hospitalini hapo kwenye Wodi Namba Tatu na kuruhusiwa
kurejea nyumbani na mtoto wake siku iliyofuata.
“Nikitoka
wodini, nilikutana na dada ambaye sikuwahi kumuona, akanisaidia kubeba
mizigo michache niliyokuwa nayo na tulipokaa kwenye benchi akaniambia
anikodie bajaj inipeleke nyumbani, tulipofika hakuteremka kwenye bajaj
akaahidi kuja tena kututembelea,” alisimulia Bishaliza.
Alisema
juzi jioni, dada huyo alifika nyumbani kwao akiwa amevaa dera na
kujitanda kikoi kizito chenye rangi ya kijani na chungwa bivu, baadaye
mama yake Bishaliza, alimpelekea chakula kisha akamuacha na mdogo wake,
Rahel Leganga (12), mtoto na mgeni wao huyo.
Rahel
alilieleza kwamba wakati wakila chakula, mgeni ambaye baada ya mama
Teddy kuondoka alijifungua ushungi aliokuwa amejifunika sehemu kubwa ya
uso wake na kumwagiza ampe vikombe ili awawekee juisi.
“Alitoa
juisi ya boksi ile inayouzwa Shilingi 3,000, akanimiminia dada kikombe
cha nusu lita na mimi akaniwekea, nilipoonja nikahisi chungu nikaikataa,
lakini dada akanywa yote,” alisimulia Rahel na kuendelea:
“Akaniambia
ninywe ili niongeze damu mwilini, nikitaka nisisikie uchungu ninywe
haraka haraka kama maji, nikamwambia mimi siinywi, tulipomaliza kula tu
dada akasema anahisi usingizi, akalala.”
Rahel
alisema hata yeye baada ya kula na kurejesha vyombo mahala pake,
alilala na alipoamka saa 11:00 alfajiri ya jana, alishangaa kumkuta dada
yake amelala fofofo huku mtoto na mgeni wakiwa hawamo chumbani.
Alisema
baada ya dada yake kuamka, walijaribu kutoka nje, lakini ilibainika
mlango ulifungwa kwa nje, majirani walisaidia kuufungua baada ya wao
kupiga kelele wakiomba msaada, yeye (Rahel) alikwenda kumuita baba na
mama yao wanaoishi mtaa wa pili.
Baba
na Mama Teddy wakiwa nje ya wodi namba 17 alimolazwa mtoto wao huyo,
walisema kati yao hakuna anayeweza kumtambua mwizi wa mjukuu wao,
isipokuwa Rahel aliyesema akimuona mwanamke huyo atambua.
Baba Teddy aliyejitambulisha kwa jina la Job Leganga, alieleza
kuwa
Teddy hana mume bali alipata ujauzito na kutokana na nyumba yao kuwa
ndogo, waliamua kumpangishia chumba mtaa wa pili kutoka nyumbani kwao
ili waendelee kumhudumia kwa mahitaji yake muhimu.
Teddy
alitaja jina la baba wa mtoto wake kuwa ni Christian Francis, ambaye
hata hivyo, aliondoka mjini hapa na kurejea kwao mkoani Morogoro.
MAJIRANI WASIMULIA
John
Nadoo (50), Mjumbe wa Nyumba Kumi katika eneo analoishi Teddy, alisema
juzi jioni alimuona mwanamke akiwa amevaa dera, amejitanda mtandio wake
kiasi cha kubakiza sehemu ndogo ya sura yake, lakini hakumsalimia badala
yake alionekana akiita watoto.
“Baada
ya kuzungumza na watoto, niliona akiongozana na mtoto mmoja, sikuelewa
kilichoendelea mpaka asubuhi nilipopata taarifa kutoka kwa majirani kuwa
mtoto wa Teddy ameibwa jana (juzi) usiku,” alieleza Nandoo.
Eunice
Shaibu (11), alisema: “Aliniita akaniuliza kwa Teddy wapi?” nikamwambia
subiri nikuitie mwenzangu akupeleke mimi nimeachwa nilinde nyumba,
nikamuita Therezia ndiye aliyempeleka.”
Terezia
Michael (11), alisema alipofika nyumbani kwa Teddy, walimkuta akiwa
amekaa kwenye kizingiti cha mlango wa kuingia kwenye ua wa nyumba yao
akampokea mkoba.
Rosemary
Ndahani (21), anayeishi chumba kilichopakana na Teddy, alisema akiwa na
mpangaji mwenzao, Happy, waliona Teddy akiingia kwenye ua wa nyumba yao
na dada anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 28, mrefu, mweupe mwenye
unene wa wastani, alivaa dera ambalo mtandio wake aliutumia kujifunga
ushungi.
Alisema
hawakufahamu kilichoendelea mpaka asubuhi aliposikia Teddy na mdogo
wake wakipiga kelele za kuomba msaada, kufunguliwa mlango wa chumba chao
uliokuwa umefungwa kwa nje na kwamba alipotoka chumbani humo alikuwa
akiweweseka mithili ya watumiaji wa dawa za kulevya.
“Alichokuwa
akitamka ni kudai mtoto wake, akisema ‘wameniibia mtoto wangu, lakini
alikuwa hajiwezi, akiweweseka kwa kukosa nguvu kabisa mpaka wazazi wake
walipofika na kumpeleka hospitali,” alieleza Ndahani.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alipoulizwa na mwandishi wa
habari hizi kuhusiana na tukio hilo, alisema analifanyia kazi na kwamba
hawezi kuthibitisha kama mtoto huyo ameibwa ama la.
No comments:
Post a Comment