Tumshukuru
Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kuonana tena wiki hii tukiwa wazima.
Lakini pia tumshukuru kwa kutuletea kitu kinachoitwa mapenzi.
Mapenzi yamekuwa yakichukua nafasi kubwa sana katika maisha yetu ya
kila siku na yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa furaha kwa kila mtu.
Kama
huamini, angalia wale waliotokea kupenda na wao wakapendwa, utabaini
nyuso zao zimetawaliwa na furaha isiyo na kifani. Lakini mapenzi hayo
hayo yamekuwa ni chanzo cha vilio kwa baadhi ya watu.
Mpenzi
msomaji wangu, kupenda hakuna macho! Moyo ukishapenda hausikii la
kuambiwa. Katika hili ndiyo maana unaweza kumuona mwanaume au mwanamke kazimika kwa mtu ambaye hawaendani kabisa lakini moyo wake ndiyo umeshapenda.
Ilishawahi
kutokea msichana akampenda kijana mmoja ambaye ni fukara kupita
maelezo. Yeye akawa ndiyo anamhudumia kwa kila kitu. Akamfanyia mpango
wa ajira na mwisho wake wakafunga ndoa.
Sasa hivi wanaishi maisha
ya furaha na amani. Wamegeuka mfano wa kuigwa kwa jinsi wanavyopendana
lakini huko nyuma msichana huyo alikuwa akichekwa kwa kutoa penzi kwa
mwanaume asiye na mbele wala nyuma.
Hayo ndiyo mapenzi jamani!
Lakini pia katika kufurukuta kumtafuta mpenzi wa kuwa naye maishani,
mwanaume au mwanamke unaweza kujikuta unaangukia kwa mtu ambaye tayari ana mpenzi
wake.
Moyo wako unakuambia yeye ndiye mtu sahihi katika maisha yako lakini tayari ana mtu wake, unafanyaje?
Utapambana
kuhakikisha unapata kile ambacho moyo wako umekipenda au utakubaliana
na ukweli kwamba huwezi kuwa naye kwa kuwa ana mtu wake? Inapofikia
hatua hiyo unaweza kujikuta upo njia panda hasa pale ambapo huyo mwenye
mtu wake naye anaonesha kuwa na chembechembe za mapenzi kwako.
Kuna mambo kadhaa ya kukusaidia kukabiliana na hali hii.
Chunguza
Tumia
muda wako mwingi kuchunguza juu ya uhusiano wake. Uhusiano wao
umesimama na wanaonekana ni watu wenye ‘future’? Nasema hivyo kwa
sababu, yawezekana uhusiano wa huyo uliyetokea kumpenda ni wa kuzuga tu
na huenda wewe ndiye mwenye ‘future’ naye. Ndiyo maana nikasema chunguza
uhusiano wake kwanza.
Usitafute uadui
Baada ya kuchunguza,
ukibaini kwamba uhusiano wao hauko ‘siriasi’, vuta subira, lolote
linaweza kutokea na likaufurahisha moyo wako. Lakini kama utaona ni watu
walio siriasi na wanaelekea kuoana, usitafute uadui bure, kaa pembeni.
Una nafasi kwake?
Sawa
umetokea kumpenda msichana aliye na mtu wake, umeshawahi kujiuliza kama
una nafasi ndani ya moyo wake? Anaonesha dalili fulani za kukupenda
kama unavyompenda na ni mtu anayeonesha kukumisi anapokuwa mbali na
wewe? Utakapobaini una nafasi kwake, uamuzi wa kumpotezea hautakuwa na
nafasi.
Ni rahisi kubadili uamuzi wake?
Unadhani huyo
uliyetokea kumpenda anaweza kubadili maamuzi ya kumuacha huyo aliyenaye
kama kweli hawana ‘future’? Utagundua hilo kwa kuongea naye na kumsikia
kama anaweza kufanya maamuzi hayo ili awe na wewe.
Pingana na moyo wako
Ifike
wakati upingane na moyo wako. Unajua moyo wako kukuambia kuwa unataka
kuwa na uhusiano na demu ambaye tayari ana mpenzi wake wakati mwingine
utakuwa unakupotosha.
Kwa hiyo ukiona vipi, pingana nao. Acha
kumng’ang’ania msichana mwenye mpenzi wake licha ya ukweli kwamba,
huenda wewe ndiye mwenye nafasi ya kuwa mume wake na siyo huyo aliye
naye.
Urafiki ni poa?
Umempenda sana na hauko tayari kumkosa
katika maisha yako lakini imetokea kwamba tayari yuko na mtu na umebaini
huna nafasi kwake kabisa? Usiumie, omba angalau urafiki. Siyo urafiki
wa kivile sana ila angalau pale unapotaka kusikia sauti yake kwa
kumsalimia tu, upate nafasi hiyo.
Usiumie, yupo mwingine
Haina
haja ya kujitafutia vidonda vya tumbo bure kwa kuwa tu umebaini
uliyetokea kumpenda tayari ana mtu. Chukulia ni hali ya kawaida, mademu
wazuri ambao wanaishi singo wapo kibao huko mtaani, ni suala la wewe
kutulia tu. Amini yupo mwingine ambaye atayafanya maisha yako yawe ya
furaha.
Naomba nihitimishe kwa kusema kwamba, unapotokea kumpenda
mtu fulani, pambana kuhakikisha unampata kwa sababu ukimkosa maisha
yako yanaweza kuwa gizani. Ila pale utakapoona uwezekano wa kuwa naye
haupo, usilazimishe ndugu yangu. Kumbuka haya ni maisha tu!
No comments:
Post a Comment