Ilikuwa Oktoba 7 mwaka huu, saa 1.00 asubuhi katika eneo la
Mbondole, Kata ya Msongola, Wilaya la Ilala mkoani Dar es Salaam
kulipozuka tafrani baada ya mwanamume mmoja kukamatwa akituhumiwa
kumweka kinyumba binti mwenye umri wa miaka 15.
Mama wa binti aliyewekwa kinyumba, Amina Juma
anasema mshtuko alioupata baada ya kumwona binti yake akichomoza katika
chumba cha mwanamume huyo, ulisababisha tumbo lake kumkata kwa uchungu.
“Sikuamini macho yangu kumuona mwanangu akitolewa
katika chumba hicho, nilitamani iwe ndoto... lakini ilikuwa kweli na
tukio hilo liliniumiza sana,” anasema mwanamke huyo.
Akisimulia huku machozi yakimtoka, anasema siku
hiyo alipata taarifa kutoka kwa mdogo wake kuwa mwanaye anaishi na
mwanamume huyo huku akifungiwa na kufuli ndani kwa kuhofia isijulikane.
Baada ya kupata taarifa hizo, walishirikiana na
mdogo wake kwenda kutoa taarifa katika ofisi ya Serikali za Mtaa huo,
ili waweze kumdhibiti mtuhumiwa na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria.
Katika ofisi hiyo, walisaidiwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi ya mtaa
huo, ambao walikaa kuanzia saa moja asubuhi hadi saa 8:30 mchana ili
kuhakikisha mtuhumiwa huyo anakamatwa.
Mkasa ulivyoanza
Ilikuwa Agosti mwaka huu mama huyo akiwa nyumbani
kwake alifika kijana mmoja ambaye alijitambulisha kuwa ni mshenga
anayetaka kutoa posa kwa mwanaye. Hata hivyo, alimkatalia na kumweleza
kuwa mtoto wake bado anasoma.
“Baada ya kumkatalia mshenga huyo akaanza kutumia
mwanya wa kuja gengeni kwangu, ili amrubuni akubali kuolewa na huyo
mwanamume lakini alikuwa anakataa,”anaelezea mama wa mtoto huyo.
Anasema siku moja mtuhumiwa alifika nyumbani kwake
na kumweleza kuwa atahakikisha mwanafunzi huyo anafutwa shule, kwa kuwa
amekwamisha mpango wake.
“Siku hiyo mtuhumiwa aliniongelea maneno ya ovyo,
nilikasirika na kuamua kuingia ndani kulala... nilipoamka sikumkuta
binti yangu.
“Nilijaribu kuwauliza majirani kama wamemwona, lakini sikupata
jibu hivyo nililazimika kwenda kwa mtuhumiwa ili kumwangalia,” anasema.
Alipofika eneo hilo alimkuta kijana mmoja na
kumuuliza kama mwanaye ameonekana lakini alimjibu hakumwona, wakati huo
aliiona baiskeli ya mtuhumiwa huyo akiwa nje ikiashiria kuwa alikuwa
ndani.
Anasema wakati alipokuwa anamwuliza kijana huyo, mara mtuhumiwa alitoka nje na baadaye alifuatia mwanaye.
Anasema kitendo hicho kilimuudhi na alimua
kumwadhibu kwa kumchapa fimbo ndipo mtoto huyo alipotoroka na kwenda kwa
baba yake mzazi ambaye anaishi Kivule, Wilaya ya Ilala.
Anasema siku ya pili alilazimika kwenda kumfuata ili wafanye kikao cha ndugu kuhusiana na suala hilo.
Baada ya kikao mtoto huyo alipoulizwa, alidai kuwa
hataki tena shule.. “hivyo nilimchukua na kwenda naye nyumbani, lakini
mume wangu wa sasa (baba mlezi wa binti huyo) alimkataa kutokana na
tabia zake.”
Siku iliyofuata alilazimika kumrudisha kwa baba yake mzazi na kuwa tangu hapo hakujua tena taarifa zake mpaka lilipotokea hili.
“Mimi naona huu ulikuwa ni mchezo uliopangwa na
mtuhumiwa na baba mzazi wa mtoto huyu, inaonekana alikuwa anajua mchezo
mzima. Kama mwanaye hakuwapo nyumbani kwa nini hakutoa taarifa polisi?
Au kwa ndugu?” anahoji.
Sakata latinga polisi
“Oktoba 10 mwaka huu nikiwa nyumbani kwangu,
walikuja askari kutoka Kituo cha Polisi Stakishari, Ukonga walichukua
maelezo yangu na ya mtoto na baada ya hapo waliniambia niende polisi
baada ya siku tatu,” anasema.
Baada ya kutoa maelezo polisi ilifunguliwa jalada
la kesi ya ubakaji lenye namba STK/RB/13749/14 na wakati huo nilipewa
fomu ya polisi kwa ajili ya kwenda Hospitali ya Amana ili vichukuliwe
vipimo vyote.
“Hivi unavyoniona nampeleka mwanangu katika Hospitali ya Amana ili akapime vipimo vyote ambavyo vinahitajika,” anaeleza.
Alivyomlea mwanaye
Mama huyo anasema aliachana na mumewe wa kwanza
wakati binti huyo akiwa na umri wa miaka miwili na kwamba tangu wakati
huo, alimlea peke yake kwa hali na mali.
Anasema alipofikisha umri wa miaka saba, alianza
darasa la kwanza na hapo akaanza kumtembelea baba yake na hata kulala
lakini hakuwahi kupewa fedha kwa ajili ya shule.
Binti anena
Binti huyo anasema alikutana na mwanamume huyo
alipokuwa anakwenda kununua mkaa katika banda lake lililopo katika eneo
hilo la Kigezi.
Anasema mwanamume huyo alikuwa akimlaghai kwa kumwambia kuwa ameshakuwa mtu mzima hivyo aache shule aolewe.
Akiwa kwa baba yake mzazi, binti huyo anasema
mwanamume huyo alikuwa akivizia baba huyo anapoondoka naye anamfuata na
kumweleza kuwa anataka kumpeleka mshenga, lakini baadaye alimtorosha.
“Nilianza kuishi naye mwezi uliopita, alinitorosha
kutoka Kivule kwa baba yangu mzazi na kunipeleka nyumbani kwake
Mbondole,” anasimulia.
Anasema wakati huo alimweleza kuwa ana watoto watatu wanaotakiwa kulelewa kwa kuwa aliachana na mama yao.
Mwanamume aliyekuwa anaishi naye alikuwa anafanya
biashara ya kuuza mkaa eneo la Kigezi na kila siku alikuwa akimwachia
Sh5,000 kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Viongozi wa Serikali wafunguka
Mjumbe wa Kamati ya Ulinzi wa Mtaa huo, Julius
Meng’anya anasema baada ya kupewa taarifa hizo walikwenda hadi kwenye
nyumba hiyo ili kumkamata mtuhumiwa. Walifika asubuhi eneo kwa ajili ya
kulinda na kuhakikisha mtuhumiwa huyo wanamdhibiti na ilipofika saa 8.30
mchana aliporudi nyumbani kwake walimkamata pamoja na mwanafunzi huyo.
Baada ya kumkamata walimtaarifu mwenyekiti wa
serikali ya mtaa huo ambaye alifika kwenye eneo hilo lakini cha
kushangaza alimwachia huru mtuhumiwa huyo.
“Kwa kweli kitendo cha mwenyekiti kumwachia
mtuhumiwa huyo kilituudhi sana tulitegemea mtuhumiwa angechukuliwa hatua
za kisheria,” anasema Meng’anya.
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Salum
Matangula alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa alikiri
mbele ya kikao kuwa alipewa ruhusa na mama mzazi wa mtoto huyo ili aishi
naye.
Anasema kutokana na maelezo ya pande zote,
walibaini kuwa wote wana makosa ndipo walipomtaka mama huyo aende kwenye
duka la dawa ili achukuliwe kipimo cha mimba na baada ya hapo ampeleke
mwanafunzi huyo shuleni.
“Niliwaeleza kuwa wote wana makosa, mama alikuwa
anadai mwanaye akapime kwanza, nikamruhusu, lakini sijapata majibu hadi
leo,” anasema Matangula.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kigezi anayosoma
mtoto huyo, Joseph Kalungutu anasema mwanafunzi huyo ni mtoro na kipindi
cha nyuma alikuwa akihudhuria darasani mara moja moja na lakini kuanzia
Septemba, mwaka huu, hakuonekana kabisa shuleni.
“Mahudhurio yake ni mabaya, baada ya kuona
maudhurio yake siyo mazuri nilimwita mama yake ambaye alidai kuwa hayupo
anaishi kwa baba yake mzazi,” anasema Kalungutu.
Anasema Septemba mwaka huu akiwa shuleni hapo
alikwenda mwanamume aliyejitambulisha kuwa mzazi wa binti huyo akidai
kuwa amekwenda hapo kwa ajili ya kumfuta shule mwanaye kwa kuwa
anaonekana mkubwa.
“Nilimkatalia na kumweleza kuwa sheria hairuhusu
mwanafunzi yeyote aliyeandikishwa kufutwa shule hadi hapo atakapomaliza.
Nilimweleza kuwa yeyote anayejaribu kufanya hivyo lazima afikishwe
kwenye vyombo vya sheria.
Mwanamume anayedaiwa kumtorosha binti huyo, Halifa Ally anakiri
kuwa aliishi naye... “Sina cha kukueleza zaidi ya hayo ninachofahamu
huyo binti nilikuwa naishi naye,” anasema Ally.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki
anasema Ally anayetuhumiwa kuishi na binti huyo ametoroka... “lakini
polisi inawahoji mama wa mtoto huyo pamoja na mwanaye katika Kituo cha
Polisi cha Stakishari huku tukiendelea kumtafuta mtuhumiwa ili afikishwe
kwenye vyombo vya sheria,” anasema Nzuki.