Michezo kadhaa ya kufuzu kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika imefanyika hii leo Novemba 15 katika viwanja tofauti barani.
Michezo hiyo ambayo ni ya pili kutoka
mwisho katika hatua ya makundi ya kufuzu imetoa timu kadhaa ambazo
zimefuzu kushiriki michuano ya AFCON ambayo itafanyika nchini Equatoria
Guinea.
Katika michezo hiyo timu ya taifa ya
Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ imefanikiwa kufuzu baada ya kuwafunga
Sudan katika mchezo uliopigwa jijini Durban kwenye uwanja wa Moses
Mabhidha .
Afrika kusini ilishinda mchezo huo kwa
matokeo ya 2-1 kufuatia mabao yaliyofungwa na Thulani Serero na Tokelo
Rantie . Sudan walijipatia bao lao pekee kwenye dakika ya 76 mfungaji
akiwa Salah Ibrahim ambaye aliingia kwenye kipindi cha pili.
Afrika kusini wamefanikiwa kufuzu kama
washindi wa makundi baada ya kukusanya pointi 11 kutokana na kushinda
mechi 3 na kutoka sare kwenye mechi mbili, huku kundi ‘A’ timu ya taifa
ya Nigeria ilifanikiwa kuwafunga Congo Brazaville 2-0 katika mchezo
uliofanyika Port Noire .
Matokeo haya yanawafanya Nigeria
kufikisha pointi 7 sawa na walizo nazo Congo Brazzavile na Nigeria
watalazimika kungoja mpaka siku ya mwisho ya kufuzu ili kujihakikishia
nafasi ya kutetea ubingwa wao kwani watategemea matokeo ya mchezo kati
ya Congo Brazzavile na Sudan.
Katika michezo mingine Cameroon
waliwafunga Congo DRC 1-0, huku Ivory Coast wakiwafunga Sierra Leone 5-1
. Gabon na Angola walitoka sare ya 0-0 na Burkina Faso wakashinda
mchezo wao dhidi ya Lesotho kwa 1-0, Zambia ambao walikuwa ugenini
Msumbiji walishinda mchezo wao dhidi ya wenyeji kwa matokeo ya 1-0 kwa
bao lililofungwa na mshambuliaji wa Tp Mazembe Given Singuluma.
Uganda waliwafunga Ghana 1-0 matokeo
ambayo yanawafanya washike nafasi ya pili kwenye kundi lao na kwa
matokeo haya timu za Afrika Kusini , Cameroon , Tunisia , Burkina Faso ,
Algeria , Gabon , na Cape Verde zimeungana na wenyeji Equatorial Guinea
kama timu zilizofuzu huku timu nyingine zikilazimika kungoja mpaka siku
ya mwisho ya michezo ya kufuzu ili kukata tiketi ya kwenda huko Malabo
ambako michuano ya Afcon 2015 itafanyika.
Facebook Blogger Plugin by Bongo na Matukio
Post a Comment