Maendeleo ya teknolojia yamebadilisha
mambo mengi katika maisha yetu ya kila siku. Zamani ilikuwa kama kuna mwanamke
au mwanaume unampenda, basi lazima uhangaike sana mpaka utakapopata nafasi ya
kuzungumza naye, na kama huna ujasiri wa
kumtongoza ana kwa ana basi ndiyo umemkosa.
Siku hizi mambo yanamalizwa
kidijitali. Kama umezidiwa na upweke, hata kama hujui kutongoza, zipo mbinu
nyingi za kisasa zinazoweza kukurahishia, kuna simu za mikononi, kuna mitandao
ya kijamii na njia chungu nzima hivyo huna haja ya kuendelea kuumia na upweke.
Ni matumaini yangu kuwa mada hii ambayo
iyaegemea zaidi katika matumizi ya simu za mkononi itakusaidia wewe ambaye
unampenda mtu fulani na lengo lako si kumchezea bali kuanzisha naye maisha ya
kifamilia.
Kumbuka kuwa penzi bora ni lile ambalo
wawili huanza kwa kuwa marafiki, ni makosa kukurupuka kumtongoza mtu kwenye
simu au kwenye mitandao ya kijamii bila kumvuta kwanza karibu yako.
Hatua ya kwanza, ukishapata namba ya
simu ya huyo umpendaye, tafuta muda ambao utakuwa umetulia kisha mpigie na
jitambulishe. Mweleze kwamba umempigia simu kumjulia hali, kama akikuuliza
mahali ulikoipata namba yake, unaweza kumjibu vyovyote lakini inashauriwa kuwa
siyo vizuri kumtajia aliyekupa namba yake kwa sababu unaweza kuwagombanisha.
Usiwe na papara, mtakie siku njema na
endelea na shughuli zako nyingine. Unaweza pia kuendelea kumtumia meseji za
kawaida (siyo za mapenzi), ukimjulia hali, ukimuuliza kama ameshakula au
amekula chakula gani, anafanya nini kwa muda huo na vitu anavyovipenda sambamba
na vile asivyovipenda.
Endelea hivyo kwa muda, siri kubwa
ambayo huijui ni kwamba watu wengi, hasa wanawake huwa wanapenda kujua kuwa mtu
fulani anamjali kwa kumuuliza mambo mbalimbali yanayohusu maisha yake ya
kawaida. Jitahidi kuwa mcheshi lakini usizidishe masihara. Ukishafanikiwa
kumvuta karibu yako na kumfanya aamini kwamba huwa unamfikiria mara kwa mara,
sasa unaweza kupiga hatua moja mbele kwa kufanya yafuatayo:
MBINU ZA KUMTEKA
Tumia sauti ya utulivu yenye hisia
ndani yake, utazidi kumvuta karibu yako. Usipende kuzungumza kwa sauti ya juu
au kupayuka au kupiga simu ukiwa kwenye kelele. Akipokea tu simu yako, mjulie
hali yake kisha msifie kidogo kuhusu sauti yake na namna anavyozungumza.
Msimulie kidogo kuhusu siku yako
inavyokwenda, tumia maneno machache lakini yatakayomfanya asiboreke
kukusikiliza. Ifanye stori yako iwe ya kuvutia kwa kutumia maneno matamu
yatakayomfurahisha na kumfanya aache kila anachokifanya na kukusikiliza.
Badili mazungumzo, muulize kama anajua
kwamba yeye ni mzuri sana na hujawahi kukutana na mtu anayevutia kama yeye.
Kama wewe ni mwanaume na unayezungumza naye ni mwanamke, utakuwa katika nafasi
nzuri ya ‘kum-win’ kwa sababu wanawake wengi wanapenda sana kusifiwa.
Akiwa amekolea na sifa unazomwagia,
mweleze kwamba unavutiwa naye na unatamani kuwa na mpenzi anayefanana naye.
Zungumza naye kwamba atakapokubali kuwa na wewe, utamtunza na kumlea kama
malkia, mweleze malengo yako ya baadaye katika uhusiano wenu endapo
atakukubalia.
Usimpe nafasi ya kukwambia kama
amekubali au amekataa bali hitimisha mazungumzo yenu kwa kumtakia siku njema au
kazi njema. Bila shaka utamuacha akiwa na shauku kubwa ya kuendelea kusikiliza
‘mistari’ yako.
Endelea kuwasiliana naye kwa mambo ya
kawaida huku ukimpima kama yale uliyomwambia anayachukuliaje. Kama naye
amekupenda, utaanza kuona mabadiliko kuanzia meseji atakazokuwa anakutumia,
namna anavyopokea simu yako na uchangamfu anaokuonesha.
Kama bado haoneshi dalili zozote za
kukuelewa, basi jua hajavutiwa na wewe na ukiendelea kuzungumzia mambo ya
mapenzi, huenda ukaanza kumboa lakini kama ana dalili za kuingia kwenye kumi na
nane zako, endeleza mawasiliano naye, omba kukutana naye sehemu tulivu kama
ufukweni au popote ambapo mtakuwa wawili na hapo utakuwa na nafasi nzuri ya kueleza
kwa kina juu ya hisia zako.
Endapo atakubali kukutana na wewe,
basi hiyo ni hatua nzuri sana kuonesha kwamba unaelekea kufanikiwa. Jambo la
msingi ni kuanza kujiandaa kwa ajili ya kukutana naye kwa sababu mwonekano wako
wa kwanza mbele ya macho yake ndiyo utakaompa sababu ya kukuchagua au
kukukataa. Kwanza anza kwa kufanya kitu ambacho huwa kinakufurahisha na
kukuweka kwenye mudi nzuri kama kuimba, kucheza muziki, kufanya mazoezi au
chochote unachokipenda sana.
Baada ya hapo, hakikisha nguo zako ni
safi, jipulizie manukato mazuri, piga mswaki, jitengeneze nywele zako vizuri na
hakikisha kila kitu mwilini mwako ni kisafi. Pangilia mazungumzo kati yako na
umpendaye kabla hata hamjakutana, hii itakuongezea kujiamini.
Hakikisha sehemu mnayoenda kukutania
kwa mara ya kwanza unaifahamu vizuri na imetulia vya kutosha. Baada ya hapo,
muandalie zawadi ndogo mfano chokleti, mkufu au ua zuri. Usihangaike kutafuta
zawadi kubwa kwa sababu siyo muhimu mnapokutana kwa mara ya kwanza.
Muda utakapowadia, wahi kufika eneo
mlilopanga kabla ya mwenzako, hii itamfanya akuheshimu zaidi kwa sababu atajua
hubahatishi mambo. Msalimie kwa uchangamfu kisha mkaribishe sehemu ya kukaa.
Jitahidi kupunguza maneno mengi badala yake zungumza kwa staha na muda mwingi
msikilize yeye. Muulize kinywaji au chakula anachokipenda kishe muagizie.
Kama wewe ni mwanaume, mkishamaliza
kunywa au kula, lipa bili hata kama yeye anao uwezo wa kulipa. Ukweli ambao
wengi hawaujui, wanawake wanapenda zaidi kuhudumiwa hata kama wana utajiri
mkubwa kiasi gani.
Mkishamaliza, uwanja ni wako sasa wa
kueleza hisia za ndani ya moyo wako. Zungumza kwa busara na kwa utulivu, huna
haja ya kupaniki kwa sababu mpaka amekubali kukutana na wewe, tayari una
asilimia kubwa ya kumpata hivyo punguza woga. Jitahidi kumtazama kwenye macho
yake unapozungumza naye, hii itakuongezea ujasiri.
Naam! Baada ya hapo naamini utakuwa
umeutua mzigo mzito uliokuwa nao, usimlazimishe kukupa majibu hapohapo endapo
ataomba umpe muda. Baada ya hapo, tayari utakuwa umefanikiwa kumvuta kwako kwa
asilimia tisini, ongeza ukaribu zaidi na utaona matokeo yake kwa sababu
hataweza kukataa ombi lako na mwisho mtatimiza lengo lenu la kufunga ndoa na
kuishi pamoja siku za mbele.
Facebook Blogger Plugin by Bongo na Matukio
Post a Comment