Tunakutana tena kupitia safu hii namba moja kwa kuandika makala kali zinazogusa maisha yetu ya kimapenzi. Ni matumaini yangu kwamba u-mzima na kwa wale wakristo wenzangu nina imani mnaendelea vyema na maandalizi ya Sikukuu ya Christmas.
 
Mpenzi msomaji wangu, tunaukaribia mwaka mpya wa 2015. Endapo tutakuwa miongoni mwa wale watakaouona mwaka huo tukiwa wazima, kwanza ni lazima tumshukuru Mungu.
Tutakuwa na kila sababu ya kufanya hivyo kutokana na ukweli kwamba, kuna ambao licha ya leo kuwa wazima wanaweza wasiuone mwaka huo na yawezekana kabisa kati yao wamo mimi na wewe! Tumuombe Mwenyezi Mungu atujalie tuwe kati ya wale watakaouona mwaka huo wakiwa wazima.
Endapo dua yetu itakubalika, tutakuwa na kila sababu ya kuhakikisha tunayaangalia upya maisha yetu ya kimapenzi. Tutatakiwa kufanya hivyo kutokana na ukweli kwamba, mapenzi yana nafasi kubwa katika maisha yetu ya kila siku.
Kwa maana hiyo endapo tutaingia mwaka mpya tukiwa na wapenzi ambao ni ovyo hata maisha yetu kwa mwaka huo yatakuwa ya ovyo. Hivyo basi, itakuwa ni jambo la busara kila mmoja kujiangalia na kuona kama mpenzi uliye naye anafaa au hafai kuingia naye katika mwaka huo.
Natambua wapo ambao mwaka 2014 umekuwa ni mchungu kwao. Wapo waliotoa machozi na kujuta kwa nini walipenda. Wapo waliokosa kabisa muda wa kuyafurahia maisha na wapenzi wao. Muda wao mwingi umekuwa ni wa huzuni huku wakiziona chembechembe za furaha kwa mbali sana.
Hii yote yawezekana ni kwa sababu waliingia katika mapenzi na watu ambao si sahihi. Huenda ulitokea kumpenda sana mtu flani ukiamini na yeye anakupenda lakini kwa bahati mbaya ukakuta tofauti, hiyo huwatokea wengi na wala si jambo la ajabu.

Lakini sasa umeshabaini kwamba umempenda mtu ambaye hana mapenzi na wewe, kuna sababu gani ya msingi ya kuendelea kumpa nafasi katika moyo wako? Unadhani ukimuacha utakufa au maisha yako yatayumba?
Elewa kwamba, kuendelea kumng’ang’ania mtu wa dizaini hiyo hakutakuwa na faida yoyote badala yake utakuwa unajiongezea matatizo ambayo mwisho wa siku utalia na asitokee wa kukufuta machozi.
Ndugu zangu, ulimwengu wa sasa si wa kutafuta heshima ya kwamba una mpenzi au una mume hata kama hana vigezo vya kuwa naye. Nasema hivyo nikiwa na maana yangu.
Kuna baadhi ya wanawake ambao licha ya kwamba wapo katika uhusiano wa kimapenzi na wanaume ambao ni wakorofi, wasio na mapenzi ya kweli kwao, bado hawako tayari kuwakosa eti tu kwa sababu wanasema, kuwa na mtu ni heshima kuliko kuitwa ‘nungayembe’.
Kwa dhana hiyohiyo ndiyo maana ukijaribu kuchunguza utagundua kuwa, wanawake wengi walio katika uhusiano wa kimapenzi iwe wameolewa au wako katika uhusiano wa kawaida, wanavumilia mengi kutoka kwa wapenzi wao hata katika yale ambayo hawastahili kuyavumilia. Ukiwauliza watakuambia hawako tayari kuishi peke yao.
Mwanamke atakuwa tayari kuvumilia kipigo anachokipata kutoka kwa mumewe kila siku eti kwa sababu hataki kuikosa ile heshima ya kwamba ni mke wa mtu.
Wapo wasichana ambao wapenzi wao wanaonesha wazi kutowajali, kutowaheshimu na kuwafanyia kila aina ya vituko lakini wanavumilia eti kwa sababu wanahisi wakiachwa wanaweza kukosa wengine wa kuwapenda.
Jamani, hebu tujiulize, kuna raha gani ya kuwa na mpenzi ambaye hukupi kile ambacho ulikitarajia kutoka kwake? Mapenzi ni furaha na ukiwa na mtu ambaye hakupatii furaha hiyo, huyo si wa kumpa nafasi katika mwaka huu ujao, muweke pembeni huku ukiamini kuwa, kumuacha kwako ndiko kutampa nafasi yule mwenye mapenzi ya dhati kuwa na wewe.
Uhusiano wako
kwa mwaka 2015
Hakikisha unaingia mwaka 2015 ukiwa na mpenzi sahihi, mpenzi ambaye atakusaidia katika kutimiza yale ambayo umepanga kuyafanya kwa mwaka huo.
Mpenzi ambaye amekuwa akichukua muda wako mwingi kumfikiria kutokana na mambo anayokufanyia, huyo si wa kumpa nafasi kabisa.
Yule ambaye amekuwa akikuliza na kujikuta unashindwa kutimiza majukumu yako, unatakiwa kumpa mkono wa kwa heri ili uwe huru kufanya mambo yako huku ukisubiri yule ambaye atakuwa na nia njema na wewe.
Kikubwa katika maisha yako ni kujiamini. Jikubali wewe mwenyewe na amini wewe si mtu wa kuchezewa na kuyumbishwa na mtu asiye na mapenzi na wewe. Amini kwamba hata bila huyo anayelipiga teke penzi lako maisha yako yanaweza kuwepo tena ya furaha zaidi. Ukijijengea imani hiyo, ni lazima utachukua uamuzi sahihi. Ni hayo tu kwa leo

Soma Nafasi za kazi na ajira bofya hapa chini kutizama, Mjulishe na mwenzio

Facebook Blogger Plugin by Bongo na Matukio

Post a Comment

 
Top